MOTTO:
VIJANA NA KAZI
**************************************
Matikiti maji hulimwa kama zao la biashara katika sehemu nyingi
duniani zenye hali ya hewa ya joto la wastani. Zao hili lina wapatia watu
shughuli za kufanya na hivyo kuwapatia kipato kuanzia kwenye nyanja za uzalishaji
hadi kwenye matumizi. Matikiti maji ni
mojawapo ya jamii aina ya matunda au mbogaboga inayotambaa. Mimea hii inapatikana katika kundi
linalojumuisha mimea mingine kama kama
matango,maboga na maskwash. Zao
la tikiti maji ni mojawapo ya zao ambalo
lina faida kubwa sana ukilinganisha na mazao mengine kwa muda mfupi.
Katika shamba la ukubwa wa shamba la ekali moja(1.acre)
lililoandaliwa vizuri, kupandwa na
kuhudumiwa vizuri mkulima ana uwezo wa
kuvuna kiasi cha TANI 15-36, ambacho kitamsaidia kupata fedha zitakazo msaidia
katika mahitaji yake mbalimbali na kuondokana na Umasikini.
HALI YA HEWA
Mimea hii husitawi katika maeneo yenye joto la wasitani yaani
haihimili hali ya joto kali sana,baridi kali, mvua nyingi na udongo
unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu. Matikiti hukua vizuri katika maeneo yenye
joto la wastani wa nyuzi kati ya 21-30 sentigradi. Iwapo mitikiti itapandwa katika maeneo yenye
joto chini ya nyuzi 15 za sentigrade huchelewa kuota
Mvua: kwa upande wa mvua
matikiti yanahitaji kiasi cha mvua kati ya millimita 400-600 kwa msimu. Mvua
nyingi husababisha uwepo wa magonjwa ya fungusi na bakiteria ambayo huathili
mavuno.
HALI YA UDONGO
Huhitaji udongo wenye rutuba nzuri ulio na virutubisho. Vile
vile haihitaji udongo wenye kiasi kikubwa cha tindikali na alikali kubwa.
Hali ya udongo katika
kipimo cha pH iwe kati ya 6.0 na 7.0. Ingawa mmea una uwezo vile
vile wa kuhimili kwenye udongo wenye pH 5.0
MAENEO YANAYOFAA KWA
KILIMO CHA MATIKITI MAJI TANZANIA.
Kwa upande wa Tanzania Inastawi vizuri kwenye ukanda wa pwani na
miinuko kidogo kama DSM, Tanga, Morogoro, Mtwara, lindi na Pwani
ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi
wa tatu mpaka wa tisa.
UANDAAJI WA SHAMBA
Kabla ya kupandikiza udongo utifuliwe vizuri na majani yaondolewe
kabisa.Shamba liandaliwe vizuri kwa kusafisha ili kuondoa mimea mingne ambayo
inaweza kuwa ni chanzo cha magonja.
UPANDAJI
Katika shamba la ukubwa wa hecta moja kiasi cha kilo 3-4 cha mbegu
kinaweza kutumika. Panda mbegu 2 au 3 moja kwa moja katika kila
shimo. Usipande katika kitalu kwasababu miche ya mitikiti huwa ni dhaifu
sana wakati wa upandikizwaji iwapo itapandwa kwenye kitalu hivyo kupelekea kufa
kwa miche hiyo. Panda umbali wa sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa
sentimeta 30 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 - 2 kutoka mstari hadi mstari.
Zingatia kutokutumia mbegu za tikiti uliloninua kwasababu linaweza kuwa ni
chotara (Hybrid) ambayo hupelekea kushusha kiasi na ubora wa matikiti yatakayo zaliwa kwa
sababu yatakuwa ni kizazi cha pili (F2)
UPUNGUZAJI WA MIMEA
Mimea ya matikitimaji huanza kuota, baada ya kama wiki 2.
Hivyo katika Mbegu mbili ulizopanda kata
moja na uache ule mche wenye afya zaidi ndio uendelee kukua.
Angalizo: using’oe mche bali ukate ili kuzuia kusumbua mizizi ya mche
uliobaki. Vilevile unaweza kupandishia udongo kwenye mashina ili kusaaidia
kupunguza maji kutuama kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi badala ya
kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na kuongeza
rutuba.
Kama una sehemu ndogo ya
shamba unaweza kuyawekea matikiti waya ya kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa
sababu ya kuhimili uzito wa matunda.
Wakati mimea inapo anza
kutambaa kwenye waya ni lazima uifundishe (kuielekezea ) kwenye waya na
kuifungia.
MATANDAZO (MULCHES)
Matandazo ina maana ya
kutumia nyasi na mabaki ya mimea mingne
kufunika aridhi. Baada ya miche
kutambaaa kwa kiasi unaweza kuweka matandazo (mulches) ambayo yaweza
kuwa nyasi kavu kwenye udongo ili kuzuia
upotevu wa unyevu vile viile kupunguza uotaji wa magugu shambani kwako. Vile vile matandazo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo
na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.
UWEKAJI WA MBOLEA
Mbolea za viwandani aina ya NPK au mbolea zenye nitrogen kiasi cha gram 10 hadi 20 ziwekwe
wakati mimea ikiwa ni midogo mpaka pale maua ya kike yatakapoanza
kuonekana. Vilevile samadi inaweza
kuwekwa wakati mimea ikiwa midogo. Baada ya mimea kutengeneza matunda weka
mbolea aina ya urea na potassium hadi mara 2 au 3 kwa wiki mpaka matunda
yatakapokomaa.
UMWAGILIAJI
Shamba linatakiwa limwagiliwe mara kwa mara wakati mvua
zinapokosekana au wakati wa mvua chache.
Kipindi muhimu zaidi ambapo mimea hii huhitaji maji ni katika kipindi
cha uotaji wa mbegu, wakati wa kutoa maua na siku takribani kumi kabla ya
kuvuna. Iwapo kutakuwa na ukosefu wa maji kutasababisha kutengenezwa kwa
matunda ambayo si mazuri na yenye umbo baya wakati wa utengenezaji wa matunda
pia upunguaji wa ukubwa wa tunda.
Angalizo; usimwagilie matikiti wakati wa jioni sana au usiku kwasababu
inaweza kusababisha magonjwa ya majani kutokana na unyevu kukaa muda mrefu. Vile
vile usimwagilie juu ya maua wakati wa
asubuhi au join kwasababu unaweza kuzuia wadudu kama nyuki ambao ni muhimu sana
wakati wa uchavushaji.
MAUA NA MATUNDA
Matikiti hutoa maua dume na
jike kwenye tawi moja. Kwa kawaida maua dume
huwa ni madogo zadi na hutoka
mapema zaidi yakifuatiwa na maua jike ambayo huwa makubwa zaidi. Maua yanaweza
yasionekane au yasitokee iwapo kiasi kidogo cha maji kitamwagiliwa ,upungufu wa
viritubisho kwenye udongo na hali ya hewa ya joto/baridi sana n.k
Uchavushaji hufanya na wadudu na iwapo itaonekana hakuna wadudu
unaweza kuchavusha kwa kutumia mkono.
Hii hufanywa kwa, kukata maua dume kwa kisu na kufanya uchavushaji
kwenye maua jike, maua jike ya mwanzo kwenye tawi ndiyo yenye ukuaji bora
zaidi, unaweza kukata tawi lisiendelee kukua baada ya matunda kutokeza hii
husababisha kuwa na matunda makubwa zaidi. Hii inawezwa kufanywa zaidi wakati
wa Asubuhi.
MAGONJWA NA WADUDU
Wadudu wa matikiti wako wa
aina mbalimbali na wanaoshambulia sehemu wanaoshambulia majani na maua, na
wengine hushambulia matunda , pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia
mimea. Magonjwa kama Ukungu wa unga (powdery mildew) na wa chini (Downy mildew)
na mengine yathibitiwe kabla hayajaleta madhara kwenye mimea.Ili kujua dawa za
magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na
pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi. Dawa aina ya Mancozeb inaweza
kutumiwa kuthibiti ugonjwa magonjwa hayo hapo juu.
Vilevile matikiti hushambuliwa na wadudu ambao hukaa katika
majani, maua na matunda. Dawa aina ya
KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda.
MAVUNO
Mavuno ya matikiti yanategeme huduma za shamba pamoja na hali ya
hewa. Matikiti pia hutofautiana katika
mavuno kulingana na aina ya matikiti. Kwa wastani matikiti yanaweza kutoa kutoa
mavuno kati ya TANI 15-36 kwa hekta
moja. Ili kujua matikiti
yamekomaa inahitaji ujuzi kidogo, upande wa chini wa tunda huanza kuwa na rangi
ya njano, pia kikonyo juu ya tunda hukauka kabisa na kuwa kijivu, ila njia
nzuri ni kuyapiga kwa kiganja na kusikiliza mlio wake kama tunavyofanya kwenye
mafenesi, hii nayo ni shule nyingine. Tumia kisu wakati wa kuvuna matikiti,
yabebwe na kuhifadhiwa vizuri kwenye makasha tayari kuuzwa au kwa matumizi
binafsi.
SOKO LA MATIKITI MAJI
Ukubwa wa tikiti na mwonekano wake ni baadhi ya sifa
zinazoangaliwa na wananuzi. Matikiti madogo sana huwa hayapendi sana na
wanunuzi. Kwa Tanzania wakulima wengi wanauza matikiti katika masoko ya ndani
yanayopatikana takribani nchi nzima. Kwa miaka kadhaa tikiti moja limekuwa likiuzwa kwa wasitani wa shilling 1000 kwa
tikiti dogo mpaka 3000 kwa tikiti kubwa katika masoko.
Mwisho
|
“UKITAKA UTAJIRI UTAUPATA
SHAMBANI”
Diaspora Company Ltd
No comments:
Post a Comment